Platini kuwa bosi wa Fifa?

Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini anatarajiwa kupata uungwaji mkono mkubwa na mashirikisho ya soka kwa ajili ya kuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Platini amekuwa akipigiwa chapuo kuchukua nafasi inayoshikiliwa na Sepp Blatter kwa miaka mingi, lakini akawa kimya hadi alipofunguka na kusema atawania. Tayari Chama cha Soka (FA) cha England limetangaza kumuunga mkono.

Platini alimshauri Blatter aachie ngazi, muda mfupi kabla ya uchaguzi wa Fifa, lakini bosi huyo, raia wa Uswisi alikataa na kusema haingewezekana. Siku nne baada ya kuchaguliwa kwake, Blatter alitangaza kwamba angejiuzulu kwani alihisi haungwi mkono na ulimwengu wa soka.

Platini anasema kwamba anataka kurejesha heshima ya shirikisho hilo ambalo limegubikwa na tuhuma nyingi za rushwa, na viongozi wake wanakabiliwa na mashitaka ya wizi, rushwa na utakatishaji fedha.

Mwenyekiti wa FA, Greg Dyke amesema kwamba anaamini Platini, mwanasoka mahiri wa zamani wa Ufaransa, akichukua anfasi hiyo atafanya mageuzi sahihi yanayotakiwa na kuondoa madoa yote. Maofisa saba wa Fifa na wengine saba wanashitakiwa nchini Marekani kwa makosa mbalimbali.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Februari 26 mwakani ambapo Blatter ataendelea kukalia kiti hicho. Mwingine anayetarajiwa kuwania uongozi ni Prince Ali Bin al-Hussein wa Jordan aliyepambana na Blatter kisha akajitoa katika ngwe ya mwisho. Amekuwa akimtaka Blatter kuachia ngazi wakati huu badala ya kuendelea kukaa ofisini.

Mwingine aliyekwishatangaza kutaka kiti hicho ni Rais wa FA ya Liberia, Musa Bility. Wengine wanaoweza kuwania nafasi hiyo ni Jerome Champagne na Chung Mong-joon.

Comments