Man U wamtaka Ronaldo

Manchester United wanaendelea na harakati zao za usajili na sasa wanafikiria kazi ngumu ya kumsajili mchezaji wao wa zamani, Cristiano Ronaldo.

Louis van Gaal anataka kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya kutafuta ubingwa msimu ujao ambapo inaelekea kikosi chao kitabadilika sana.

Imefika miaka sita sasa tangu Ronaldo (30) aondoke Old Trafford kwenda Real Madrid kwa ada ya pauni milioni 80, akiweka rekodi ya dunia alipouzwa na Sir Alex Ferguson.

United wameshasajili wachezaji Memphis Depay, Matteo Darmian, Bastian Schweinsteiger na Morgan Schneiderlin. Kadhalika wamewaondoa Radamel Falcao, Robin van Persie na Nani.

Sasa wanataka kumpata Ronaldo na wengine wanasema watamsajili Zlatan Ibrahimovic kutoka Paris Saint-Germain (PSG). Kuna uwezekano wa kumuuza Angel di Maria kwa PSG, mchezaji aliyevunja rekodi ya usajili England kwani alilipiwa pauni milioni 59.7.

United waliulizia uwezekano wa kumsajili Ronaldo kiangazi kilichopita walipokuwa na kocha David Moyes lakini mchezaji huyo alisaini mkataba mpya na Los Blancos hadi 2018.

Kuna tetesi kwamba Ronaldo haelewani na kocha mpya, Rafa Benitez, hivyo Man U wanachukulia upenyo huo ili kumsajili. Amepata kueleza mapenzi yake kwa United na hata akiwafunga bao huwa hashangilii.

United pia wanataka kumsajili mshambuliai wa Barcelona, Pedro, 27, ambaye ameshawaeleza klabu kwamba anataka kuondoka kwa sababu hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, Madrid wamewaambia kwamba watatakiwa kulipa pauni milioni 22 kama ilivyo kwenye masharti ya mkataba wake wa usajili.

Bado United wanaendelea kumsaka mlinzi wa kati wa Madrid, Sergio Ramos japokuwa Madrid wanang’ang’ania abaki. Madrid nao wamesitisha harakati za kumsajili kipa Mhispania, David De Gea kutoka Manchester United.

Comments