Marekani yaomba kupelekewa

watuhumiwa wa mlungula Fifa

Marekani imetuma maombi rasmi kwa Uswisi kwa ajili ya kuwasafirisha hadi kwake maofisa saba wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) waliokamatwa jijini Zurich Mei mwaka huu, ili wakakabiliane na mashitaka ya rushwa.

Maombi rasmi yaliwasilishwa Jumatano hii, ambapo maofisa hao saba ni miongoni mwa 14 wanaodaiwa kuhusika na kupokea rushwa, wizi na utakatishaji wa fedha. Mashitaka hayo yamefunguliwa baada ya uchunguzi wa kina uliendeshwa na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

Kabla ya kukubali au kukataa ombi hilo, polisi wa Uswisi watawapa maofisa hao fursa ya kusikilizwa na kujibu hoja mbalimbali, ambapo maofisa na wanasheria wao wana siku 14 za kujibu maombi hayo, ambapo ikiwa kuna sababu za msingi watahamishiwa Marekani.

Wanadiplomasia wa Marekani ndio waliwasilisha maombi ya kupelekewa maofisa hao na maombi yalifikishwa kwenye wizara ya sheria. Inaelezwa kwamba maofisa wote wamepanga kukata rufaa, mchakato utakaokwenda hadi Mahakama ya Juu ya Uswisi na si ajabu ukachukua miezi kadhaa.

Njia nyingine za kujinasua na hali hiyo ni kukubali moja kwa moja kwenda Marekani, ambako wataweka mawakili, waombe dhamana na pia wawatetee katika kesi ya msingi. Uswisi inadaiwa kuwachukulia maofisa hao kwamba wanaweza kuruka dhamana hivyo hawatapewa.

Tangu wakamatwe katika hoteli yenye hadhi ya nyota tano kabla ya uchaguzi wa rais wa Fifa, maofisa hao wapo rumande. Maofisa wanaoshikiliwa ni Mkuu wa Shirikisho la Soka la Amerika na Caribbean (Concacaf), Jeffrey Web, Mkuu wa Shirikishola Soka la Costa Rica, Eduardo Li, Eugenio Figueredo wa Uruguay, Rafael Esquivel wa Venezuela, Jose Maria Marin wa Brazil, Ofisa Maendeleo wa Fifa, Julio Rocha wa Nicaragua na Costas Takkas ambaye pia ni kiongozi wa Concacaf.

Comments