ROBO FAINALI CONCACAF

Paraguay wawatoa Brazil

Michuano ya Copa America imerudia historia yake ya 2011 baada ya
Paraguay kuwatoa Brazil kwa mikwaju ya penati.
Kwa ushindi huo, Paraguay watakutana na Argentina kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Mshambuliaji wa zamani wa Manchester City, Robinho alifunga bao la
Brazil katika dakika ya 15 akitia nyavuni majalo ya Dani Alvez.
Ilikuwa mechi ya 99 ya mkongwe huyo Robinho, lakini mambo yalibadilika pale Thiago Silva alipounawa mpira na kumruhusu Derlis Gonzalez kusawazisha kwa penati.

Wakati hadi mwisho wa muda wa kawaida mambo yalikuwa 1-1, Brazil
walikosa nafasi mbalimbali. Kutolewa huko kwa Brazil kumesitisha
‘ufufuko’ wa timu hiyo iliyo chini ya Dunga.

Brazil walifanya vyema kwenye mechi nyingi zilizopita baada ya fainali
za Kombe la Dunia 2014 nchini mwao, ambapo waliadhiriwa kwa kufungwa mabao 7-1 na Ujerumani kwenye nusu fainali.

Brazil hawajapata kutwaa ubingwa wa michuano hii tangu 2007 huku
Paraguay wakiwa na fursa ya kurudia waliyofanya 1979.

Paraguay watacheza na Argentina Julai mosi wakati katika nusu fainali
nyingine Chile ambao ni wenyeji watakutana na Peru Julai 4.
Robinho (31) alicheza badala ya Neymar ambaye amefungiwa kwa utovu wa nidhamu uwanjani. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Robinho kufunga kwenye soka ya ushindani tangu 2010.

Comments