Mkwasa kocha mpya Stars

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ameteuliwa kuwa Kocha wa Taifa Stars.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametangaza kwamba kocha huyo ataendelea pia na majukumu yake Yanga lakini atakapohitajika Stars atakuwa huko.

Mkwasa anachukua kwa muda nafasi ya Mdachi Mart Nooij aliyefutwa kazi baada ya timu kufungwa kwa mara yingine 3-0 majuzi.
Malinzi alipeleka barua wizarani kuiomba serikali kama ilivyokuwa inamlipa Nooij ifanye hvyo kwa Mkwasa, ambapo mshahara ulikuwa dola 12,500.

Stars walilala 3-0 mbele ya Uganda katika Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar kwenye mechi ya kutafuta kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2016.

Kabla ya hapo walifungwa idadi hiyo hiyo ya mabao na Misri katika mechi ya kufuzu kwa mashindano ya Afrika (AFCON) 2017.

Mkwasa atasaidiwa na Hemed Morocco, ambapo Malinzi aliwashukuru Yanga na Mafunzo ya Zanzibar kwa kuridhia makocha hao kuchukua nafasi hizo katika uzalendo wa kusukuma mbele gurudumu la soka.

Mkwasa atatafuta benchi lake la ufundi kwa ajili ya kuendelea na mashindano ya AFCON na CHAN ambapo Tanzania ina wakati mgumu kutokana na kupoteza mechi za awali. Pia Stars walipoteza mechi zote tatu walipoalikwa Afrika Kusini kwa michuano ya COSAFA.

Katika mechi zake 18 Nooij ameshinda tatu tu, kufungwa tisa na sare sita.

Comments