Zambia wabadili kocha

Kocha wa klabu ya Zesco ya Zambia, George Lwandamina ameteuliwa kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Zambia – Chipolopolo.

Lwandamina anachukua nafasi ya Honour Janza lakini atashika nafasi hiyo kwa muda, kwani imeelezwa kwamba anayetakiwa kushika nafasi hiyo moja kwa moja ni kocha wa kigeni.

Hatua hiyo imekuja siku tano tu kabla ya mechi baina ya Zambia na Guinea Bissau kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017.

Janza aliwaongoza Zambia kwenye fainali za AFCON mwaka huu nchini Guinea ya Ikweta na uteuzi umekuja siku moja tu baada ya Janza kuwaongoza Chipolopolo kuwafunga Ethiopia bao 1-0 kwenye mechi ya kirafiki.

Hata hivyo, Janza amepewa majukumu mapya ya kuwa mkuu wa programu za maendeleo ndani ya Chama cha Soka cha Zambia (Faz) wakati chama hicho kikiendelea kutafuta kocha wa kudumu.

Taarifa za kutafutwa kocha wa kigeni kwa ajili ya Chipolopolo zilipotolewa, Janza alieleza alijihisi kusalitiwa na Faz kwa sababu taarifa zilitolewa kwa wengine kabla ya yeye kujulisha.

Hata hivyo, Faz wamesema kwamba bado Janza ni mtu muhimu katika mipango ya chama hicho na kwamba baada ya tafakari ya kina wameona haja ya kupata kocha wa kigeni kuwavusha.

Comments