VURUGU ZA SOKA MISRI

Adhabu ya kifo palepale

Mahakama nchini Misri imeshikilia uamuzi wa adhabu ya kifo kwa washitakiwa 11 waliohusika na fujo zilizosababisha mauaji kwenye dimbani katika jiji la Port Said 2012.

Machafuko hayo yalitokea katika mechi baina ya klabu za Al-Ahly na Al-Masry Februari mwaka huo, ambapo washabiki 74 wa soka walipoteza maisha.
Hizo zilikuwa vurugu kubwa zaidi zilizosababisha maafa makubwa katika historia ya soka nchini Misri.

Hukumu hii imekuja wakati wa kupitiwa upya kwa kesi iliyokuwa ikiwakabili washitakiwa 73.

Kati yao washitakiwa 40 walipewa adhabu ya vifungo vya hadi miaka 15 jela wakati wengine waliachiwa huru. Bado uamuzi huu unaweza kupingwa katika mahakama ya juu.

Vurugu hizo zilitokea baada ya mechi, ambapo washabiki walivamia uwanjani na kuanza kuwashambulia washabiki wa Al-Ahly kabla ya wapinzani wao nao kuvamia. Vifo vilitokana na kugongana, kukatwa na vitu mbalimbali na ukosefu wa hewa.

Katika kesi hiyo kulikuwa na maofisa wa polisi kadhaa walioshitakiwa lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyehukumiwa kifungo cha maisha. Mkuu wa usalama wa zamani wa Port Said amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.

Maofisa wa polisi walikuwa wakishitakiwa kwa kuruhusu washabiki kutoka timu mwenyeji ya Al-Masry kuwashambulia wale wa Al-Ahly yenye makao yake makuu jijini Cairo na ambao walikuwa wakiunga mkono kupinduliwa kwa Rais Hosni Mubarak.

Machafuko hayo yalisababisha vurugu nyingine jijini Cairo ambako watu 16 waliuawa. Wakati huo, Rais Mohammed Morsi alitangaza hali ya hatari.

Morsi alikuja kupinduliwa na Jenerali Abdel Fattah el-Sisi ambaye hatimaye alichaguliwa kuwa rais anayeendelea na uongozi hadi sasa.

Comments