Sunderland waokoka kushuka

*Advocaat alia kwa furaha, Arsenal wa tatu

Sunderland wamefanikiwa kwa msimu mwingine kubaki Ligi Kuu ya England, baada ya kupambana kiume dhidi ya Arsenal na kupata pointi moja muhimu waliyokuwa wakiihitaji kwa udi na uvumba.

Kocha wa muda aliyeajiriwa mahsusi kuwaokoa na kushuka daraja, Dick Advocaat amefanikisha mpango wake huo, na baada ya kipenga cha mwisho kushuhudia wakienda suluhu alitoa machozi ya furaha akishangilia na wachezaji wake.

Sunderland walicheza kwa kujilinda zaidi, wakidhamiria kutoruhusu bao na Arsenal wakicheza nyumbani Emirates walionekana kukosa makali licha ya kutawala mchezo kwa asilimia 75. Hii ni mechi ya tatu Arsenal wanashindwa kufunga bao nyumbani.

Pointi hiyo moja, hata hivyo, imewasogeza Arsenal karibu kabisa na nafasi ya tatu na hivyo kufuzu moja kwa moja Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na kuwasukumiza Manchester United kwenye mechi za mtoano za UCL.

Hii inaelekea itabaki hivi kwa sababu Arsenal wana pointi 72 na Manchester wanazo 69. Arsenal wanawazidi Man U kwa uwiano wa mabao saba, hivyo ili Man U washike nafasi ya tatu watatakiwa wawafunge Hull walau mabao saba na Arsenal wapoteze mechi dhidi ya West Bromwich Albion bila kufunga bao.

Kipa wa Sunderland, Costel Pantilimon alitokea kuwa shujaa wa mechi baada ya kuokoa hatari zilizokuwa zikielekezwa kwake na wachezaji wa Arsenal. Wamewaachia msala Hull na Newcastle.

Ili kuokoka kushuka daraja kwenye mechi za mwisho za EPL Jumapili hii, Newcastle wanatakiwa wawafunge West Ham na hiyo itakuwa salama yao. Hull walio pointi mbili nyuma ya Newcastle watatakiwa wawafunge Manchester United kwenye mechi yao ya mwisho na waombe Newcastle wafungwe au waende sare au suluhu.

Comments