Barcelona mabingwa La Liga

Barcelona wametawazwa kuwa mabingwa wapya wa Hispania baada ya kuwachapa Atletico Madrid 1-0.

Alikuwa nyota wa dunia katika soka, Lionel Messi aliyefunga bao pekee la mechi hiyo ya ugenini na kuwapa Barca ubingwa wa 23 katika historia ya La Liga.

Lilikuwa bao la 41 la Messi katika ligi, akiwa nyuma kwa mabao manne kwa Cristiano Ronaldo wa Real Madrid wanaomaliza msimu bila taji lolote.

Ronaldo alifunga mabao matatu katika mechi dhidi ya Espanyol, lakini ikiwa imebaki mechi moja moja tu kwa kila timu, Barcelona wamefikisha pointi 93 wakati Madrid wanazo 89 na Atletico 77.

Kocha Luis Enrique anawania Barca kupata mataji matatu msimu huu, ambapo baada ya kutwaa ubingwa wa nchi, wanasubiri mechi ya fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya Athletic Bilbao Mei 30 na fainali ya ubingwa wa Ulaya dhidi ya Juventus mwezi ujao.

Chini ya pep Guardiola, Barcelona walitwaa mataji matatu msimu wa 2008/9 na sasa safu yao ya ushambuliaji inatisha, wakiwa na Neymar, Messi na Luis Suarez.

Atletico Madrid ndio waliokuwa wakishikilia ubingwa wa La Liga, lakini msimu huu wamekuwa dhaifu kidogo, hasa baada ya kuondokewa na mpachika mabao wao, Diego Costa aliyejiunga Chelsea.

Barcelona watamaliza kwa mechi dhidi ya
Deportivo La Coruna walio katika hatari ya kushuka daraja. Msimu uliopita Barca hawakupata taji lolote.

Comments