Chelsea wakaribia ubingwa

 

Chelsea wamepambana hadi kushinda 3-1 baada ya kuanza nusu ya kwanza vibaya dhidi ya Leicester.

 

Mabingwa hao watarajiwa walienda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao moja lililofungwa na Marc Albringhton, ambapo ilionekana kama vile wenyeji wangewazuia Chelsea.

 

Hata hivyo, Didier Drogba ambaye alikuwa hajafunga tangu Desemba 6 alisawazisha dakika tatu tu baada ya kuanza kipindi cha pili, nahodha John Terry akatia la pili kabla ya Ramires kumaliza kazi.

 

Ilibidi vijana wa Jose Mourinho, ambao wamekuwa wakidaiwa kuegesha basi na kucheza soka isiyovutia, wabadilike na kuongeza nguvu na kiwango ili kuwazidi Leicester.

 

Hivi sasa Chelsea wanahitaji pointi tatu tu kutawazwa mabingwa, kwani sasa wanazo pointi 80 wakati wanaowafuata wanazo 67 ambao ni Manchester City na Arsenal.

 

Watacheza na Crystal Palace nyumbani Stamford Bridge Jumapili hii na bila shaka wangependa iwe siku ya kumaliza kazi jukumu la msimu kwa kupata ubingwa baada ya miaka mitano.

 

Leicester walikuwa wameshinda kwenye mechi zao zote nne zilizopita na nahodha Terry alisema kwamba Chelsea wanahitaji kuheshimiwa kwa kuweza kuongoza ligi kwa tofauti hiyo kubwa ya pointi na sasa kuelekea kwenye ubingwa.

 

Manchester United wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 65 huku Liverpool waliopigwa na Hull majuzi wakiwa wa tano na pointi zao 58 huku matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya yakizidi kutoweka.

 

Sunderland, QPR na Burnley wapo katika hatari kubwa zaidi ya kushuka daraja, lakini pia Leicester na Aston Villa, Hull na hata Newcastle wanatakiwa kujiimarisha kuondoka eneo baya.

 

Comments