Yanga mabingwa Tanzania

 

 

Yanga wametawazwa kuwa mabingwa wa soka wa Tanzania baada ya kufikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

 

Yanga ambao wamecheza mechi 24 wametwaa ubingwa huo baada ya kuwacharaza Polisi Morogoro 4-1.

 

Yanga walipata mabao yao kupitia kwa Amissi Tambwe aliyepachika matatu na Simon Msuva aliyefunga moja na pia anaongoza kwa ufungaji kwenye ligi hiyo.

 

Yanga walionesha wazi kudhamiria kutwaa ubingwa huo katika mechi za karibuni, ambapo washambuliaji wake wamekuwa wakali kama nyuki, wakishambulia malango ya wapinzani bila huruma na kufunga idadi kubwa ya mabao.

 

Yanga wametwaa ubingwa wakiwaacha Azam katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 10 huku Simba wakiwa wa tatu na pointi zao 41, zikiwa ni nne pungufu ya Azam, hivyo kuwa na nafasi finyu ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

 

Mbeya City waliokuwa hatarini kushuka daraja wamekwenda vizuri sasa, ambapo wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 31 wakifuatiwa na Kagera sugar.

 

Polisi Morogoro ndio wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kushuka daraja kwani wanashika mkia wakiwa na pointi 25 sawa na Ndanda Fc na Prisons.

 

Timu za Mgambo, Stand United, Coastal Union, Ruvu JKT na Mtibwa zote zimefungana zikiwa na pointi 28 wakati Ruvu Shooting wanazo 29.

Comments