Johnson matatani kwa kubaka

Mwanasoka wa England na Sunderland, Adam Johnson amefunguliwa mashitaka ya kufanya ngono na mtoto mwenye umri wa miaka 15.
Johnson (27) anayetoka Castle Eden, Durham, anadaiwa kufanya makosa kama hayo matatu, ambapo aliwasili Kituo cha Polisi cha Peterlee na mwanasheria wake na kuachiwa kwa dhamana.
Winga huyu aliyepata kuchezea England na ambaye bado anatarajiwa kuitwa kikosini atapanda kizimbani katika Mahakama ya Peterlee Mei 20 mwaka huu kujibu mashitaka yake.
Sunderland walikuwa imemsimamisha mchezaji wake huyu kusubiri hatima ya uchunguzi dhidi yake, lakini Machi 18 waliamua kumrejesha kikosini.
Johnson anadaiwa kufanya makosa hayo kati ya Desemba mwaka jana na Februari mwaka huu, ambapo ni makosa kufanya mapenzi na msichana aliye chini ya umri wa miaka 18 au bila ridhaa yake.
Mhusika aliyefanyiwa kitendo hicho hakutajwa na polisi, kwa sababu ya haki za binadamu na hata kesi ikianza anaweza asitajwe au kesi isikilizwe pasipo wanahabari kuruhusiwa kuhudhuria.
Johnson alizaliwa Sunderland na kuanza soka katika klabu ya Middlesbrough kabla ya kuhamia Manchester City Februari 2010 kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni saba.
Alihamia Sunderland mwaka 2012 kwa ada ya pauni milioni 10. Amecheza mechi 97 akiwa na City. Amechezea timu ya taifa ya England kuanzia ile ya U-19 hadi ya wakubwa.
Mwanasoka huyu anaelezwa kuwa na uhusiano na Stacey Founders ambaye ana mtoto naye aliyezaliwa Januari mwaka huu, muda mfupi kabla ya kudaiwa kufanya jinai inayompeleka mahakamani.

Comments