‘De Gea awakubalia Real Madrid’

 

Kipa namba moja wa Manchester United aliye kwenye kiwango cha juu, David De Gea anadaiwa kujadiliana na Real Madrid na kukubali kujiunga nao.

 

Kituo cha Televisheni cha Sexta cha nchini Hispania anakotoka De Gea na waliko Real kimeripoti kwamba kinachosubiriwa sasa ni makubaliano baina ya klabu mbili hizo.

 

Mwanahabari mahiri anayeaminika, Josep Pedrerol amenukuliwa katika kituo hicho cha televisheni akisema kwamba De Gea (24) anataka kucheza Bernabeu msimu ujao.

 

“David De Gea amewakubalia Real Madrid na anataka kuwa hapa kuanzia msimu ujao. Klabu ilitafakari njia mbalimbali za kukabiliana na suala la kipa na sasa wametulia kwa De Gea,” anasema Pedrerol na kuongeza:

 

“Moja ya vilivyokuwa vikidhaniwa vingekuwa vikwazo kwa De Gea kutua Madrid ni kipa mkongwe aliyepo, lakini kwa sasa hilo si tatizo tena.”

 

Kwa hali hii, De Gea anaweza kurudi kwenye jiji ambalo alianza kung’ara kisoka, ambapo Real ambao ni mabingwa wa Ulaya wamehusishwa naye kwa muda mrefu, hasa wakati huu mkataba wa kipa huyu na United ukielekea ukingoni.

 

Katika kipindi kinachoitwa ‘Jugones’ kilichorushwa mchana, ilidaiwa kwamba kuna uhusiano usio mzuri sana baina ya De Gea na kocha wake, Louis van Gaal.

 

De Gea aliyezaliwa Madrid alianza kuchezea timu ya vijana ya Atletico Madrid akiwa na umri wa miaka 13 na akapanda hadi kikosi cha kwanza. Kwa sasa anacheza pia Timu ya Taifa ya Hispania.

 

Kipa huyu alihamia United 2011 kwa ada ya pauni milioni 17.8 ambayo haijafikiwa na kipa yeyote Uingereza na amechezea timu hiyo zaidi ya mechi 100.

 

De Gea amechezea pia timu za taifa za vijana za Hispania kuanzia chini kuanzia chini ya miaka 15 hadi chini ya miaka 23 kabla hajaingia timu ya wakubwa.

 

Comments