Daktari Bayern Munich aangushiwa jumba bovu

Kichapo walichopata Bayern Munich cha mabao 3-1 kutoka kwa Porto kimesababisha daktari wa timu hiyo, Hans-Wilhelm Mueller-Wohlfahrt kuachia ngazi.

imageBayern waliochapwa ugenini kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) Jumatano hii wanadaiwa kumwangushia jumba bovu daktari huyo, kwa maana kwamba yeye na wasaidizi wake ndio chanzo cha kufungwa kwao.

Mueller-Wohlfahrt (72) ambaye pia ni daktari wa timu ya taifa ya Ujerumani amesema ameshangazwa na kisingizio hicho cha ajabu, na kwamba uaminifu alioujenga katika kazi hiyo na kushirikiana vyema na idara nyingine umeharibiwa.

 

Daktari huyo amefanya kazi na mabingwa hao wa Ujerumani tangu 1977, hivyo uamuzi aliochukua ni mgumu na utawatia simanzi viongozi wa klabu kwa mtu aliyekuwa kama baba hapo.

“Idara yangu imelaumiwa msingi wa timu kufungwa, zikitolewa sababu za ajabu kabisa,” akasema daktari huyo mkongwe aliyepata kuondoka klabuni hapo kwa muda mfupi alipokosana na kocha wa enzi hizo, Jurgen Klinsman.

Katika mechi hiyo, Bayern walicheza bila wachezaji muhimu — Bastian Schweinsteiger, Arjen Robben, Franck Ribery na David Alaba waliokuwa majeruhi, lakini haieleweki ni kwa kiasi gani Mueller-Wohlfahrt ana makosa haijaeleweka.

Kuna video iliyomwonesha Kocha wa Bayern, Pep Guardiola akionesha kumkasirikia mtu kwenye benchi, anayedhaniwa kuwa kocha huyo, baada ya Medhi Benatia kuumia wakati wa mechi dhidi ya Bayer Leverkusen.

Bayern walipoteza mechi kwa idadi ya mabao sawa na Paris Saint-Germain (PSG) waliochapwa na Barcelona.

Hata hivyo, pengine kwa utani, Kocha Guardiola amenukuliwa akisema kwamba pamoja na kusikitishwa na kichapo walichopata, yeye bado ni mtu mwenye furaha. Hakufafanua maneno hayo na huenda ndiye amechangia daktari kufikia uamuzi wa kuachia ngazi.

Comments