Penati iliyorudiwa siku tano baadaye

 

England na Ulaya wameweka historia baada ya penati kurudiwa siku tano baada ya ile ya awali kukataliwa.

 

Hiyo ilikuwa kwenye mechi ya kufuzu kwa michuano ya Ulaya baina ya England na Norway kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 19.

 

Alikuwa ni beki wa Arsenal, Leah Williamson aliyefunga penati ya kwanza jijini Belfast, lakini mwamuzi wa Ujerumani, Marija Kurtes akakataa bao lililotokana nayo.

 

Mwamuzi aliamua kwamba wakati akipiga penati hiyo, wachezaji wenzake waliingia kwenye eneo la 18, lakini kisheria, ingetakiwa aamuru penati irudiwe.

 

Kinyume chake, Kurtes aliamuru upigwe mpira wa adhabu dhidi ya England, wakati ambapo walikuwa nyuma kwa bao 2-1.

 

Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) liliingilia kati na kuamuru penati hiyo irejewe siku yano baadaye na Williamson tena akaipiga na kufunga hivyo England wakafuzu.

 

Katika mechi hiyo, England walikuwa wamepewa penati hiyo katika dakika za majeruhi. Ili kufuzu walitakiwa pia kuwafunga Uswisi, jambo walilofanya kwa kuwafunga 3-1 na sasa watashiriki kwenye fainali zitakazofanyika nchini Israel.

Mwanamama huyo wa Washika Bunduki wa London alisema kwamba baada ya kukataliwa kwa penati yake ya awali alisikitika, hakuwa na la kufanya bali kwenda kulala na hakuwa na hamu ya kuipiga tena.

 

Mama yake alifanikiwa kubadili siku ya kusafiri kwa ndege ili ashuhudie bintiye akirudia kupiga penati hiyo. Mwamuzi Kurtes aliondolewa kwenye kazi hiyo kutokana na makosa aliyofanya.

 

England na Norway wanaungana na Sweden,Ufaransa, Ujerumani, Hispania na wenyeji Israel kwenye fainali hizo zinazoanza Julai 15.

Comments