Liverpool waponea kwa Rovers

Liverpool wamefanikiwa kuingia nusu fainali ya Kombe la FA baada ya kuwafunga Blackburn Rovers 1-0.

Wakiwa wametoka kupigwa 4-1 na Arsenal kwenye Ligi Kuu wikiendi iliyopita na kufifia matumaini ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, Liver walipata bao kupitia kwa Philippe Coutinho.

Mchezaji huyo wa Brazil alifunga pia kwenye mechi ya marudiano na Bolton katika raundi ya nne na sasa vijana hao wa Brendan Rodgers watachuana na Aston Villa katika Uwanja wa Wembley.

Hata hivyo, bado Liverpool hawakuonesha kiwango kikubwa kwenye mechi ya Jumatano hii, na yaweza kuonekana kwa nini walipoteza mechi zake dhidi ya Manchester United na Arsenal.

Nusu fainali ya kwanza ya FA ni baina ya Reading na Arsenal Aprili 18 na siku inayofuata ndipo Liver watacheza na Villa.

Kipa wa Liverpool, Simon Mignolet aliyeanza msimu chini ya kiwango aliokoa mabao mawili ya wazi kutoka kwa Tom Cairney na Ben Marshall.

Dakika za mwisho alimzuia kipa wa Rovers, Simon Eastwood aliyekaribia kufunga mpira wa kona.

 

Comments