Morocco waibwaga CAF kortini

*Ni kuwazuia kushiriki AFCON
Morocco wameibuka kidedea kwenye rufaa yao dhidi ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lililowafungia miaka miwili kushiriki michuano yake.
Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) limetupilia mbali uamuzi wa CAF wa kuzuia taifa hilo la Afrika Kaskazini kushiriki michuano ya AFCON 2017 na 2019.
CAF walitoa adhabu hiyo baada ya Morocco kuzira kuandaa fainali kama hizo mwaka huu katika dakika za mwisho, na CAF kuokolewa na nchi ndogo ya Guinea ya Ikweta walioyaandaa kwa mafanikio makubwa.
Guinea wenyewe awali walitupwa nje ya michuano hiyo na CAF kwa madai ya kuchezesha mchezaji asiye na sifa kwenye mechi za kufuzu, lakini walipoamua kuokoa jahazi wakaondolewa kifungoni.
Katika uamuzi wake, CAS pia imepunguza adhabu kwa Morocco kulipa faini, ambapo badala ya kulipa pauni 675,000 sasa watalipa pauni 34,000 tu.
Hata hivyo, uamuzi wa CAF kuliagiza Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) kulipa fidia ya pauni milioni 5.8 kutokana na kujitoa dakika za mwisho na kuingiza CAF matatani kiasi cha kukaribia kushindwa kuwa na mashindano hayo haikuondolewa.
CAS imesema kwamba fidia hiyo inaweza kupitiwa upya na mamlaka nyingine. CAF wanadai kwamba waliingia hasara kubwa kutokana na Morocco kujitoa miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.
Morocco waliomba kuahirishwa kwa michuano ili kwanza wajiweke sawa na mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola uliokuwa umezuka Afrika Magharibi, na CAF walipowakatalia Morocco wakajitoa.
Adhabu hizo zilitolewa Februari na Morocco wakasema hawakubaliani nazo zote ndipo wakakata rufaa CAS.
Baada ya ushindi huu, Makamu Rais wa FRMF, Nourredine Bouchhati amesema kwamba habari za uamuzi wa CAS ni nzuri, zinafikisha mwisho mzozo wao na CAF na sasa wataendelea kufanya kazi pamoja.
Amesema kwamba wanakutana na Kocha wa Timu ya Taifa, Baddou Zaki ili waanze mara moja matayarisho ya program zilizo mbele yao.

Posted under:  All Articles, Caf, Featured, Football, Sport, Sports, Sports News

Tags:  

Comments