KUFUZU KWA EURO 2016

Vurugu zavunja mechi ya Urusi

Vurugu kubwa zimejitokeza uwanjani na kusababishwa kuvunjwa kwa mechi ya kufuzu kwa mashindano ya Euro 2016 baina ya Urusi na Montenegro.

Dalili za fujo zilionekana mapema katika Uwanja wa Gradski ulioko Podgorica, kwani katika dakika ya kwanza tu ya mchezo, kipa wa Urusi, Igor Akinfeev alipigwa kwa fashifashi kichwani.

Katika mechi hiyo ya Kundi G, kipa Akinfeev alipigwa nyuma ya kichwa na kulazimika kutolewa nje kwa machela kwenda kupata matibabu na nafasi yake kuchukuliwa na kipa mwingine.
Mechi hiyo ilisimama kwa muda wa dakika 35, ndipo mwamuzi Mjerumani, Deniz Aytekin akauanzisha tena.

Hata hivyo, timu zikiwa bado kufungana, katika nusu ya pili vurugu zilizuka, ambapo wachezaji wa Urusi walipigana na wale wa Montenegro, ambapo watu wa benchi la ufundi nao walihusika.
Katika kipindi cha pili mchezo ulisimama kwa dakika 18 baada ya kuzuka vurugu baada ya penati ya Roman Shirokov ya dakika ya 66 kuokolewa na kipa wa Montenegro, Vukasin Poleksic.

Kutokana na vurugu kuzidi huku kukiwa hakuna dalili za utulivu wala amani, mwamuzi hatimaye aliamua kuvunja mechi hiyo.
Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) limesema kwamba linasubiri kupata ripoti ya mwamuzi na mjumbe wake kabla ya kuchukua hatua za kinidhamu.

Montenegro ambayo ilimtumia mshambuliaji wa Manchester City, Stevan Jovetic wamefungana na Urusi kwa pointi tano
Inaelezwa kwamba kipa Akinfeev alipelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi, ambapo alipata majeraha ya moto na kuumia shingo.

Comments