Brazil wawafumua Ufaransa 3-1

*Falcao atuma salamu kwa Van Gaal

Brazil chini ya kocha Dunga wameendelea kuchanua kwenye mechi za kirafiki na sasa wamewakandamiza Ufaransa kwa mabao 3-1.
Licha ya Raphael Varane kuwaongoza Ufaransa kwa bao katika kipindi cha kwanza, Neymar alisawazisha kabla ya Oscar na Luiz Gustavo kupachika la tatu.
Hiki ni kipigo cha kwanza kwa Ufaransa tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka jana huku Dunga akishikilia rekodi ya kushinda tangu ashike kazi hiyo baada ya aibu Brazil waliyopata kwao.
Katika mechi chini yake tangu Septemba mwaka jana, Brazil waliwachapa Colombia 1-0 kama walivyofanya kwa Ecuador kisha wakawafunga Argentina 2-0, wakawachakaza Japan 4-0 kisha Uturuki kwa idadi hiyo hiyo.
Brazil pia waliwafunga Austria 2-1 na sasa wamewanyuka Ufaransa, wakisubiri mechi dhidi ya Chile Machi 29 kwenye Dimba la Emirates.

FALCAO AIBUKIA COLOMBIA

Katika mechi nyingine, mshambuliaji wa Manchester United, Radamel Falcao ameibukia kwenye Timu ya taifa ya Colombia na kufunga mabao mawili, lakini dhidi ya timu dhaifu ya Bahrain.
Falcao ambaye ama hukosa namba Man U au kucheza chini ya kiwango na kutolewa, aling’ara kwenye emchi hiyo, akiwa ameshasema pia kwamba mwisho wa msimu huenda akatafuta timu nyingine ili apate muda wa kucheza mara kwa mara.
Katika mechi hiyo ya kirafiki, Falcao ambaye amefunga mabao manne tu katika mechi 22 kwa United akiwa huko kwa mkopo kutoka Monaco ya Ufaransa, amekasoro bao moja kufikia rekodi ya mabao ya raia mwenzake, Arnoldo Iguaran ambayo ni 24.
Falcao pia alitengeneza bao alilofunga Carlos Bacca, kwenye mechi ambayo Colombia walitoka na ushindi mnono wa 6-0.
Falcao alikosa fainali za Kombe la Dunia mwaka jana kutokana na kuwa na majeraha ya goti na sasa amefunga mabao 23 katika mechi 55 kwa taifa lake.
Mcolombia huyo analipwa £265,000 kwa wiki na ili Man U waendelee naye baada ya mwisho wa msimu watatakiwa kulipa pauni milioni 43.5, jambo linaloonekana halitatokea.
Katika mechi nyingine za kirafiki Iran waliwalaza Chile 2-0 huku Scotland wakiwafunga Ireland Kaskazini 1-0, Georgia wakiwazidi nguvu Malta kwa 2-0, Denmark wakawafunga marekani 3-2 na Ujerumani wakatoshana nguvu na Australia kwa 2-2.

Comments