Bilioni kwa klabu za EPL

Wakati washabiki wa soka wakipinga kupanda kwa bei ya tiketi, klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zitavuna pauni bilioni moja kutokana na dili la Ligi ya Soka na kampuni za televisheni.
Neema hiyo inakuja kwa furaha miongoni mwa klabu ambazo ni wanahisa wa Ligi ya Soka na pia klabu zimekubali kuwalipa ujira mujarab wafanyakazi wao wa kudumu.

Hali hiyo itaanza msimu wa 2016/17, baada ya Bodi ya Ligi Kuu kuuza haki ya matangazo ya televisheni kwa vituo vya Sky na BT kwa pauni bilioni 5.136 kwa mkataba wa miaka mitatu.
Mapato yameongezeka kwa asilimia 40, kutoka pauni milioni 700. Makubaliano hayo yalifikiwa kwenye mkutano wa klabu za EPL na Bodi ya Ligi Alhamisi hii.

Washabiki waliandamana mbele ya jengo la mkutano kupinga kupanda kwa bei ya tiketi, wakiona kwamba huko kunatokana na televisheni hizo kuamua kulipa donge nono ili kuziondoa kwenye ushindani wapinzani wao.

Wafanyakazi kwenye klabu husika waliokuwa wakilipwa mshahara kidogo usiowawezesha kujitegemea nao wameula, kwa sababu watalipwa kiwango kizuri, kuanzia pauni 9.15 kwa saa kwa wanaoishi jijini London na pauni 7.85 kwa walio maeneo mengine ya Uingereza.

Kulikuwa na malalamiko makubwa juu ya jinsi watumishi wa klabu kubwa za EPL wanavyoishi kifukara huku klabu zikiingiza fedha nyingi, wachezaji wakisajiliwa kwa ada kubwa na kulipwa mishahara ya kutisha.

Comments