Chelsea sare na PSG

Chelsea wamekwenda sare ya 1-1 na Paris Saint-Germain (PSG) katika mechi ya mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) hatua ya 16 bora.

Branislav Ivanovic aliwapa Chelsea bao la kuongoza dakika ya 36 wakiwa ugenini, lakini Edinson Cavani akaonesha umuhimu wake kwa kusawazisha katika dakika ya 54.

Mchezaji wa zamani wa Chelsea, David Luiz aliyeonekana kutopendwa na kocha Jose Mourinho alicheza nafasi ya kiungo kwa PSG dhidi ya timu yake yazamani, akicheza vyema. Diego Costa aliyerejea uwanjani kwa timu yake baada ya kuzuiwa kwa mechi tatu hakuonekana kuwa na makali.

Chelsea walilazimika kujihami kutokana na mashambulizi ya PSG na wataridhika kwa kuondoka Ufaransa na sare hiyo, ambapo wenyeji walitawala sana kipindi cha pili. Beki Ivanovic alifunga kwa kichwa kutokana na kufinyiwa mpira na Gary Cahill kutokana na majalo ya John Terry.

Cavani nusura afunge bao la ushindi lakini mpira wake uliotokana na pasi ya Blaise Matuidi ulikuwa mwingi. Msimu uliopita Chelsea walisonga mbele licha ya kuwa na mizania ya mabao 3-3 na PSG, wakafaidika kwa bao la ugenini. Mourinho alisema kwamba timu yake ilikuwa na bahati kuambulia sare hiyo.

Katika mechi nyingine, Shakhtar Donetsk walikwenda suluhu na Bayern Munich, ambapo kiungo wa Bayern, Xabi Alonso alipewa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya, kwenye mechi yake ya 100 ya UCL.

Mhispania huyo alimchezea vibaya Alex Teixeira kwenye mechi ambayo Bayern walikuwa ugenini katika nusu ya kwanza, lakini pia akamfanyia faulo Taison kipindi cha pili na kutolewa nje. Bayern walikosa mabao kupitia kwa Thomas Muller mara mbili, ambapo alipaisha na shuti jingine likatoka nje. Watakutana Munich, Ujerumani Machi 11 kwa marudiano.

Leo FC Basel wanawakaribisha FC Porto huku Schalke wakiwa wenyeji wa Real Madrid katika mwendelezo wa mashindano hayo makubwa zaidi kwa klabu barani Ulaya.

Comments