Misri wasitisha mechi za soka

Mamlaka nchini Misri zimesitisha mechi za ligi ya soka baada ya vurugu zilizosababisha vifo vya washabiki zaidi ya 22 katika uwanja jijini Cairo.

Washabiki walikufa na wengine kujeruhiwa kutokana na kugongana baada ya msongamano uliosababishwa na polisi kufyatua mabomu ya kutoza machozi dhidi ya washabiki wa Zamalek waliokuwa wanajaribu kuingia humo wakati wa mechi dhidi ya watani wao wa jadi jijini humo.

Rais Abdul Fattah al-Sisi ameeleza kusikitishwa kwake na tukio hilo, akaahidi uchunguzi kufanywa haraka, huku baadhi ya mashuhuda wakiwalaumu polisi kwa kulazimisha washabiki kutoka kupitia eneo finyu lililokuwa limezungushiwa wigo.

Ligi Kuu ya Misri ilipata kusitishwa Februari 2012 baada ya washabiki 74 kuuawa kwenye vurugu zilizozuka mchezo huko Port Said. Ligi hiyo ilianza tena mwaka uliofuata lakini washabiki walipigwa marufuku kuhudhuria mechi hadi Desemba mwaka jana, ambapo idadi ndogo ya washabiki wamekuwa wakiruhusiwa kuingia.

Vyombo vya habari vinasema kwamba tiketi 5,000 tu zilitolewa kwa ajili ya mechi hiyo iliyofanyika Jumapili licha ya uwanja wa Air Defense kuwa na nafasi ya kukaa watu 30,000. Maelfu ya washabiki wasiokuwa na tiketi walikuwa wakilazimisha kuingia uwanjani kwa nguvu

Comments