Guinea ya Ikweta, Kongo Kinshasa nusu fainali

Wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Guinea ya Ikweta wamevuka na kutinga nusu fainali baada ya kuwachapa Tunisia 2-1.
Guinea walio nafasi 96 chini ya Tunisia walishangaza kufanikiwa kupata ushindi, baada ya kuwa nyuma kwa bao moja bado dakika za mwisho. Tunisia walifunga kupitia kwa Ahmed Akaichi kutokana na majalo ya Hamza Mathlouthi.

Guinea walipata bao lao katika dakika za majeruhi kutokana na penati iliyotolewa na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wachezaji wa Tunisia. Ilifungwa na Javier Balboa baada ya Ali Maaloul kuadhibiwa kwa kumchezea vibaya Ivan Bolado.

Alikuwa ni Balboa alitefunga bao zuri la ushindi kwa mpira wa adhabu ndogo kutoka yadi 25. Ilibidi walinzi wampe ulinzi wa ziada mwamuzi Rajindraparsad Seechurn kutokana na kuzongwa na wachezaji wa Tunisia wakipinga uamuzi wake wa kutoa penati dakika za mwisho. Mechi hiyo ilichezwa kwa dakika 120.

Hii ni mara ya kwanza kwa Guinea ya Ikweta kufika hatua ya nusu fainali, na walikuwa wakichukuliwa kama wasindikizaji kutokana na kiwango chao cha chini cha soka. Wananchi wa taifa hilo wamefarijika kwa kuvuka huko, ikizingatiwa kwamba taifa lilibeba mzigo wa kuandaa mashindano baada ya Morocco kujitoa dakika za mwisho kwa kuhofia ugonjwa wa Ebola.

Katika mechi nyingine ya robo fainali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walifanikiwa kuwafunga jirani zao wa Kongo Brazzaville 4-2 kwenye mechi kali. Kongo Brazzaville walikuwa mbele kwa mabao 2-0 hadi dakika ya 62 kabla ya Kongo Kinshasa kuamka.

Mabao ya Kongo Brazzaville yalifungwa na Ferebory Dore na Thievy Bifouma kabla ya Dieumerci Mbokani kufunga la kwanza, Jeremy Bokila kusawazisha, Joel Kimuaki kufunga la tatu na Mbokani kutia la nne dakika ya 90.

Comments