Chelsea, Man City hakuna mbabe

Vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL), Chelsea wamekwenda sare ya 1-1 na mabingwa watetezi, Manchester City na kubakisha pengo la pointi tano baina yao
City walitawala mchezo kwa asilimia 57 lakini walitangulia kufungwa kwa bao la Loic Remy dakika ya 41 kabla ya David Silva kusawazisha dakika nne tu baadaye.

Chelsea walicheza bila wachezaji wao Diego Costa aliyefungiwa na Cesc Fabregas aliye majeruhi, huku City wakikosa huduma za wachezaji wa Ivory Coast, Yaya Toure na Wilfried Bony walio Guinea ya Ikweta kwa mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois alionekana kufanya makosa na wa kulaumiwa kwa bao la City ambao walimchezesha mchezaji wa zamani wa Chelsea, Frank Lamparad katika dakika 17 za mwisho, ambapo washabiki walimpokea kwa kumshangilia.

Jose Mourinho alimtoa mfungaji Remy na nafasi yake kuchukuliwa na beki Gary Cahill akionesha kwamba alikuwa na lengo la kuhakikisha wanalinda sare hiyo na si kuongeza mabao. Manuel Pellegrini wa City hakufurahishwa na kuambulia pointi moja.

Baada ya mechi hiyo, kocha Mourinho hakutekeleza majukumu ya kuzungumza na wanahabari na Ijumaa pia alifuta mkutano wake na wana habari kabla ya mechi hiyo. Kocha msaidizi Steve Holland naye hakuzungumza na wana habari badala yake Remy na Nemanja Matic walizungumza nao.

Katika mechi nyingine, Manchester United walipata ushindi wa pili mfululizo kwenye ligi baada ya kuwakandika Leicester 3-1, yakiwamo mabao mawili ya Robin van Persie na Radamel Falcao huku jingine Leicester wakijifunga kupitia kwa Morgan.

Liverpool walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya West Ham, ambapo Daniel Sturidge aliyerejea baada ya kuwa amjeruhi kwa muda mrefu alifunga moja, jingine likitiwa kimiani na Raheem Sterling.
Tottenham Hotspur waliwafunga West Bromwich Albion 3-0, Hull wakalala 3-0 pia kwa Newcastle, Crystal Palace wakapoteza 1-0 mikononi mwa Everton, Stoke wakawapiga QPR 3-1 na Sunderland wakawazidi Burnley 2-0.

Comments