Arsenal wavuka kihunzi FA

Arsenal wamejitofautisha na vigogo wengine wa ngazi za juu katika Ligi Kuu ya England (EPL) waliohenyeshwa na kutolewa au kulazimishwa kurudiana na timu ndogo za madaraja ya chini kwenye michuano ya Kombe la FA.

Washika Bunduki wa London, ambao ndio mabingwa watetezi, wakicheza ugenini walifanikiwa kuwafunga Brighton 3-2 kwenye michuano hiyo, na tayari Kocha Arsene Wenger amesema wao ni miongoni mwa wanaopewa nafasi kuchukua taji la msimu huu.

Ushindi huo umekuja siku moja baada ya Manchester City, Chelsea, Southampton na Tottenham Hotspur kutolewa na timu za madaraja ya chini, huku Manchester United wakienda suluhu na timu ndogo na watarudiana Old Trafford.

Winga Theo Walcott aliweka bao la kwanza kalba ya Mesut Ozil kufunga la pili, wote wakirejea kutoka kwenye majeraha. Brighton walio ligi daraja la pili (Championships) walikomboa bao moja kupitia kwa Chris O’Grady.

Hata hivyo, mchezaji mwingine aliyetoka kwenye majeruhi, Tomas Rosicky kufunga la tatu kwa Arsenal. Sam Baldock aliwafungia wenyeji la pili robo saa kabla ya mpira kumalizika, lakini halikubadilisha matokeo.

Kocha wa Brighton, Chris Hughton aliyepata kuwafundisha Norwich, alisema walijipa wenyewe mlima mkubwa wa kupanda kwa kuruhusu mabao mawili kutoka kwa timu ya kiwango kizuri kama Arsenal, lakini pia aliwapongeza vijana wake kwa kujituma baada ya hapo na kufanikiwa kupata mabao mawili.

Matokeo mengine kwa Jumapili hii yalikuwa Bristol City kulala 1-0 mbele ya West Ham, Aston Villa kuwazidi nguvu Bournemouth kwa 2-1. Leo Rochdale watapepetana na Stoke kwenye mwendelezo wa michuano hiyo.

Comments