Man United wabanwa na ‘watoto’

*Cambridge walio nafasi 76 kwa ligi nyuma ya Manchester United

Manchester United wakichezesha kikosi kilichogharimu pauni milioni 180 wamebanwa na timu ya Cambridge iliyo kwenye ngazi ya nne ya ligi chini ya United, ambayo usajili wa wachezaji wao haukuwagharimu hata senti tano.

Ilikuwa kwenye hatua ya nne ya michuano ya Kombe la FA, ambapo Man U wakiwa na kikosi cha kwanza walilazimishwa kuondoka na suluhu, hivyo kulazimisha mechi hiyo kurudiwa katika dimba la Old Trafford.

Ikipigwa kwenye Uwanja wa Abbey, mechi ilihudhuriwa na washabiki 7,987, Cambridge walio nafasi 76 kwa ligi nyuma ya Manchester United wakatumia urefu wa wachezaji wao kuwadhibiti Mashetani Wekundu, ambapo Kocha Louis Van Gaal alirudia tena kuchezesha mabeki wanne pale nyuma kuzuia uvujaji.
united flops

Washabiki wa wenyeji walishangilia kwa nguvu pale mwamuzi Chris Foy alipopulia kipenga cha kumaliza mchezo. Cambridge wanashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi. Kipa wa wenyeji, Chris Dunn alicheza vyema, akiwanyima raha akina Radamel Falcao na Angel Di Maria wakati Robin van Persie naye hakuwa na msaada wa kuleta ushindi.

Cambridge ni timu iliyojengwa upya, kwani imerejea kwenye Ligi ya Soka msimu huu, baada ya kutokuwapo kwa miaka tisa, lakini walikula sahani moja na Man United hadi mwisho. Vijana wa Van Gaal walipambana hasa kuvuka hatua ya tatu, ambapo walicheza na Yeovil.

Miashahara ya wachezaji wa Cambridge kwa pamoja ni kati ya pauni milioni moja tu wakati wale wa Manchester ni kwenye pauni milioni 200.
Kocha wa Cambridge, Richard Money alisema amefurahishwa na matokeo, wachezaji hawakuamini baada ya mechi naye amewaambia waende Old Trafford bila kuwa na wasiwasi wala kujali kitakachotokea, bali wafurahie kucheza hapo na timu kubwa walioweza kuwahimili.

Comments