De Gea: Homa inapanda homa inashuka

Dirisha dogo la usajili huenda likashuhudia makubwa, kwani bado kuna tetesi za uwezekano wa kipa wa Manchester United, David De Gea kutimkia kwao Hispania ili kujiunga na Mabingwa wa Ulaya, Real Madrid.

De Gea (24) aliye kwenye kiwango cha juu wakati huu anawindwa na mabingwa hao na katika kuwakatisha tamaa, United walisema kwamba ada yake ni pauni milioni 50, kiwango ambacho Real wakiamua watatoa.

Wakala wa mchezaji huyo, Mreno Jorge Mendes ambaye ndiye namba moja kwenye udalali wa soka, amesema kuna uwezekano wa mchezaji ‘wake’ huyo kuhamia Real. United tayari wamemsajili kipa wa zamani wa Barcelona, Victor Valdes kama kipa wao chaguo la pili.

Wakati hayo yakijiri, Man United wanadaiwa wanaandaa ofa kwa ajili ya beki wa kati wa Villarreal, Gabriel Paulista (24) ambaye tayari yupo kwenye mazungumzo na Arsenal ili ahamie Emirates.

Chelsea wanakimbizana na muda ili kufanikisha usajili wa kiungo wa Shakhtar Donetsk, Douglas Costa (24).

Kocha wa West Bromwich Albion, Tony Pulis amethibitisha kwamba ananuia kumsajili winga wa Wigan, Callum McManaman (23) na kiungo wa Manchester United, Darren Fletcher (30). QPR wanatarajia kumsajili mshambuliaji wa Corinthians, Alexandre Pato ili awanusuru kushuka daraja.

Kocha wa Swansea, Garry Monk analenga kumsajili beki wa kushoto wa Norwich, Martin Olsson (26) na kiungo wa Stuttgart, Alexandru Maxim (24).

Hull wanamuwinda winga wa Tottenham Hotspur na and England, Aaron Lennon (27) anayetarajiwa kuondoka White Hart Lane mwezi huu.

Mchezaji wa zamani wa Chelsea anayetakiwa na Arsenal na Manchester United kuimarisha eneo la kiungo, Kevin de Bruyne (23) ambaye kwa sasa yupo Wolfsburg amesema hana nia ya kurudi England.

Hatima ya kipa namba moja wa Arsenal, Wojciech Szczesny imeingia wkenye utata, baada ya kuwapo taarifa kwamba Arsenal wanafuatilia kwa karibu kipa wa Fiorentina, Norberto Neto (25).

Roma wanawashawishi Chelsea kukubali kupokea pauni 380,000 tuu ili wamchukue winga Mohamed Salah (22) kwa mkopo hadi mwisho wa msimu ujao.

Comments