AFCON 2015: Tunisia wawaadhibu Zambia

*Cape Verde wawakomalia Kongo

Tunisia wametumia ubovu wa Zambia na upotevu wao kuwaadhibu, wakati taifa lenye watu 500,000 la Cape Verde wakiwabana kwa suluhu Kongo Kinshasa wenye watu milioni 70.

Tunisia walitoka nyuma kwa bao 1-0 na kuwashinda Zambia 2-1, kwa mabao waliyofunga dakika 20 za mwisho, huku upande wa pili Cape Verde wakiwa na rekodi ya kuwa nchi ndogo zaidi inayoshiriki mashindano hayo.

Katika mechi ya Zambia, wachezaji walianza vyema kwa Emmanuel Mayuka wa Southampton kutikisa nyavu za Waarabu baada ya kupokea majalo murua ya Rainford Kalaba. Hata hivyo, Mayuka aliumia baadaye wakati akijaribu kutumbukiza mpira kwenye goli lililokuwa wazi.

Ahmed Akaichi wa Tunisia alitumia vyema mwanya uliojitokeza na kufunga bao la kusawazisha, na wakati Zambia wakiendelea na mchezo mbovu, Yasine Chikhaoui aliwafungia Tai wa Carthage bao la pili na la ushindi, hivyo kuwafanya waondoke na pointi nne katika mechi mbili.

Kocha wa Zambia, Honour Janza aliwalaumu wachezaji wake kwa uchoyo, ambapo kila mmoja alikuwa anacheza kana kwamba kuonesha kiwango chake kipo juu. Zambia wenye pointi moja na wamebakisha mechi moja wapo katika wakati mgumu.

Tangu watwae kombe hilo 2012, Zambia hawajapata kushinda mechi, wakitoka sare nne kabla ya kichapo hiki. Mayuka alikosa mabao kadhaa ya wazi.

Cape Verde wao walikula sahani moja na Kongo na kuhakikisha walau wanaondoka na pointi moja wote. Kongo walipata pigo kwa Nahodha Youssouf Mulumbu ambaye ni kiungo wa West Bromwich Albion kulazimika kutoka nje kipindi cha kwanza baada ya kubanwa na misuli ya paja lakini kipa wao, Robert Kidiaba alikuwa kivutio tosha kwa mbwembwe zake na uwezo wa kuzuia wafungaji wa Cape Verde.

Comments