MBIO ZA URAIS WA FIFA

Ginola na mapenzi ya soka

David Ginola ametangaza kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Mfaransa huyu aliyepata kuchezea klabu kubwa ya Paris Saint-Germain (PSG) na Tottenham Hotspur anasema anataka kumwondosha madarakani Rais Sepp Blatter.

Tunamjua Ginola ambaye dimbani alijulikana na kupendwa kutokana na kujiamini kwake, na mbinu za uchezaji zilizompandisha kwenye kilele cha mafanikio.

Hata hivyo, kucheza na kuongoza soka ni vitu viwili tofauti, na kwa jinsi alivyozungumza wakati akitangaza nia yake hiyo, kilikuwa kama mbingu na ardhi – ukilinganisha uchezaji wake na anakotaka kwenda.

Haonekani kuwa mtu mwenye kujua vyema masuala ya uhusiano wa umma na alipozungumza, kitu cha kwanza alichosema ni kwamba alikuwa pale kuzungumzia mapenzi.

Naam, mahaba ya soka, si ya wanadamu, akisema ni wakati wa kuanza upya soka.

“Nipo hapa leo kuzungumza juu ya mapenzi. Nipo hapa kushirikishana nanyi baadhi ya hisia kali zaidi ambazo yeyote kati yetu amewahi kuzipata.

“Hiyo ndiyo maana ya soka kwangu, kwako na kwa mabilioni ya washabiki wa soka duniani. Ndiyo maana tuna masikitiko makubwa tunapozungumzia baadhi ya matatizo yanayohusiana na jinsi soka inavyoendeshwa. Ni wakati wa kubadilika, ni zama za kuanza upya soka,” ndivyo alivyosema gwiji huyo wa soka mwenye umri wa miaka 47.

Tayari kuna tetesi kwamba Ginola anafadhiliwa kuwania nafasi hiyo kubwa zaidi katika kazi za soka duniani.
Zipo tetesi kwamba analipwa £250,000 kwa kujihusisha na kampeni hii na kwamba fedha nyingine kiasi cha £100,000 zimetengwa kwa ajili ya ulinzi wa Ginola.

Kuingia kwake kilingeni kunafanya wagombea urais kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Mei mwaka huu kufikia wanne.
Hao ni pamoja na Blatter (78) anayetetea kiti chake na anayepingwa na wengi, lakini pia kuna mwanadiplomasia Jerome Champagne kutoka Ufaransa na Prince Ali Bin Al Hussein wa Jordan.

Comments