Blatter apata mpinzani Fifa

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Prince Ali Bin Al Hussein ametangaza kuwania urais wa shirikisho hilo.
Prince Ali wa Jordan (39) , akichuana na Rais Sepp Blatter (78) anayewania nafasi hiyo kwa kipindi cha tano, akikabiliwa na upinzani mkali kutokana na tuhuma za rushwa kulighubika shirikisho.
Prince Ali amesema huu ni wakati wa kuondokana na utata wa utawala na kujielekeza kwenye masuala ya soka ili kuikuza, vichwa vya habari viwe juu ya soka na si rushwa au uongozi.

Prince Ali alichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Soka cha Jordan 1999 kabla ya kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Fifa kwa Asia 2011.

Huyu ni mmoja wa maofisa walioshinikiza kuwekwa wazi kwa ripoti ya mwanasheria Michael Garcia juu ya hali ya rushwa kwenye Fifa juu ya uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022.
Kadhalika alipambana kuondoa marufuku dhidi ya hijab kwa wanawake kwenye soka.
Anasema kwamba ameshawishiwa kuwania nafasi hiyo na rafiki zake kupitia ujumbe ambao amekuwa akitumiwa mara kwa mara, kisha akaamua kuusikiliza kwa makini na kuurudia, na kuona kwamba huu ni muda wa mabadiliko.

Comments