Balotelli matatani tena

“KWA nini mimi kila wakati?” ni swali ambalo mshambuliaji aliyetokea kuwa butu wa Liverpool, Mario Balotelli amekuwa akijiuliza hadi kuliandika kwenye fulana yake anayovaa ndani ya jezi.

Safari hii ameingia tena matatani, kwani Chama cha Soka (FA) kimemshitaki kwa makosa ya kupandisha katika mtandao wa jamii maneno yanayoonekana kuwa ya kibaguzi.

Balotelli (24) aliweka kwenye mtandao wa Instagram picha ya mhusika wa kwenye michezo ya kompyuta, Super Mario, iliyokuwa na maneno ya Kiingereza yanayomaanisha ‘anaruka kama mtu mweusi na kupokonya sarafu kama Myahudi’.

Hata hivyo, mchezaji huyo wa Timu ya Taifa ya Italia, baada ya kufanya hivyo alituma ujumbe kupitia mtandao wa Twitter akikanusha kuwa na nia mbaya kwa maneno hayo, na baada ya hapo aliomba radhi.

FA wamempa hadi saa 12 jioni ya Desemba 15 awe amejitetea, ambapo msemaji wa Liverpool amekiri juu ya uamuzi wa FA na kwamba mchezaji huyo atafuata hatua takikana kujibu mashitaka yake.

Balotelli anadai kwamba alitumia kikaragosi kilichotengenezwa na mtu mwingine, akidhani kwamba ilikuwa katika kutaniana tu, akisema si kweli kwamba weusi wote wanaweza kuruka juu sana wala kwamba Wayahudi wote wanapenda sana pesa.

Liverpool ana majeraha na amekosa mechi kadhaa, kama itakavyokuwa Jumamosi hii kwenye mechi dhidi ya Sunderland. Amefunga mabao mawili tu katika mechi zake 14 msimu huu kwa Liverpool.

Comments