Brahimi mwanasoka bora Afrika

Kiungo wa Kimataifa wa Algeria, Yacine Brahimi ameshinda Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa 2014 kama ilivyoendeshwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Brahimi (24) anayechezea Porto ya Ureno ni raia wa kwanza wa Algeria kutwaa tuzo hiyo ambayo hupigiwa kura na washabiki wa soka. Ameshinda baada ya washabiki kuvunja rekodi ya upigaji kura kutoka nchi 207 zilizosajiliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Brahimi amewashinda kipa wa Timu ya Taifa ya Nigeria, Vincent Enyeama; mchezaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang, Gervinho na Yaya Toure wote wawili wa Ivory Coast. Toure aliitwaa tuzo hiyo mwaka jana.

Brahimi amesema kwamba ni heshima kubwa kwake kupata tuzo hiyo na kwamba anaitolea kwa ajili ya nchi yake na watu wote waliomchagua, akisema pia kwamba ni kombe kwa watu wote wa Afrika.

Alisema kombe hilo litampa nguvu na ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi, kuwa mzuri ndani na nje ya dimba ili aweze pamoja na timu anazotumikia, kupata mafanikio makubwa. Msimu uliopita aling’ara sana kwa klabu na nchi yake.

Comments