Roy Keane aacha kazi Villa

Kocha Msaidizi wa Aston Villa, Roy Keane ameacha kazi mara moja klabuni hapo, alikokuwa chini ya Paul Lambert.

Keane (43) alikuwa akifanya kazi hiyo sambamba na ile ya ukocha msaidizi wa Jamhuri ya Ireland. Amedumu katika nafasi yake Aston Villa tangu Julai mwaka huu tu.

“Hatimaye kujumuisha majukumu yangu ya Villa na Ireland yameonekana kwamba ni magumu mno kubeba. Si haki kwa Villa wala Ireland kuendelea na yote mawili, hivyo nimefanya uamuzi wa kuondoka Villa,” akasema.

Kiungo huyu wa zamani wa Manchester United aliyepata kufanya kazi ya kufundisha Sunderland na Ipswich amekuwa pia na hali ngumu ya kupanga muda wake vya kutosha kwa ajili ya timu hizo na familia yake.

Lambert amesema kwamba msaidizi wake huyo alifika kwake Ijumaa hii na kumweleza ukweli kwamba maji yamefika shingoni, hivyo hawezi kuendelea na kazi Villa Park, jijini Birmingham.

Lambert alisema kwamba anaelewa na kuheshimu uamuzi wa Keane aliyesema katika muda wake mfupi alikuwa wa msaada mkubwa, lakini akasema kwamba haingewezekana aendelee na majukumu yote mawili.

“Katika muda mfupi tuliofanya kazi pamoja, amekuwa wa msaada mkubwa kwangu na naelewa sababu za kuondoka kwake na nakubaliana na uamuzi wake kabisa,” akasema Lambert ambaye timu yake iliyo pointi mbili tu juu ya eneo la kushuka daraja, wanacheza na Burnley wikiendi hii.

Walifurushwa kwenye michuano ya Kombe la Ligi na Leyton Orient walio Ligi Daraja la Kwanza na ambao hawafanyi vizuri huko.

Comments