Guinea wenyeji AFCON 2015

Katika hali ya kushangaza, Guinea ya Ikweta iliyokuwa imefutwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2015, imeteuliwa kuwa nchi mwenyeji na timu yake itashiriki.

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limefikia uamuzi huo baada ya waliokuwa wawe wenyeji, Morocco kukataliwa ombi la kuahirishwa michuano hiyo kutoka Januari 17 hadi Februari 8 mwakani kwa hofu ya kusambaa kwa maradhi hatari ya Ebola yaliyoua zaidi ya watu 5,000 Afrika Magharibi.

Rais wa CAF, Issa Hayatou ametangaza uamuzi huo baada ya kukutana na Rais Teodoro Obiang jijini Malabo, Guinea Ijumaa hii na rais kukubali serikali ya taifa lake kubeba msalaba huo.

Guinea walioandaa michuano hiyo pamoja na Gabon 2012 sasa watakuwa wenyeji pekee, na walikuwa wametolewa katika hatua za awali kwa madai ya kuchezesha mchezaji asiyekuwa na sifa walipocheza na Mauritania Mei 17 mwaka huu.

Morocco wametupwa nje ya mashindano hayo moja kwa moja, itabidi wajipange upya kwa ajili ya kufuzu kwenye inayokuja. Mashindano ya mwakani yanashirikisha timu 16.

“Mkuu wa Taifa la Guinea ya Ikweta amekubali kuwa mwenyeji wa michuano hiyo, kwa hiyo Kamati ya Utendaji ya CAF inatangaza kwamba mashindano yataendelea kama yalivyopanga na Guine ya Ikweta itashiriki kama nchi mwenyeji.

“Caf inapenda kutoa shukurani zake za dhayi kwa watu wa Guinea ya Ikweta, serikali yao na kwa namna ya pekee Rais Obiang,” akasema Hayatou kwenye taarifa yake.

Mechi zitachezwa katika miji ya Bata, Ebebiyin, Mongomo na mji mkuu wal Malabo. Mwaka 2012 ni viwanja vya Malabo na Bata tu vilitumiwa. Droo kwa ajili ya fainali hizo zitapangwa Malabo Desemba 3.

Comments