City wawakong’ota Manchester United

*Smalling kadi nyekundu, Rojo majeruhi

Kocha Louis van Gaal ameendelea na masikitiko yake, baada ya timu yake kuchapwa na Manchester City 1-0 katika mchezo uliotawaliwa na ubabe.

Manchester United licha ya kufungwa na kupoteza pointi tatu, waliwapoteza wachezaji wawili, Chris Smalling aliyelambwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya na Marcos Rojo aliyeumia bega na kutolewa nje kwa machela.

United walikuwa wakicheza na timu isiyo imara sana katika siku za karibuni, kwani ushindi wa City ni wa kwanza katika mechi nne zilizopita, bao lao likifungwa na Sergio Aguero. City walifungwa na West Ham kwenye mechi iliyopita na kudungwa na Newcastle waliowatoa kwenye michuano ya Kombe la Ligi.

Wachezaji wengi walionesha utovu wa nidhamu na ilikuwa bahati kwamba ni kadi moja tu nyekundu ilitolewa na mwamuzi Michael Oliver. Man City walilalamika zaidi kwamba walinyimwa penati za wazi kadhaa.

United sasa wapo nafasi ya 10 wakiwa na pointi sawa na West Bromwich Albion, Everton na Newcastle licha ya kwamba wametumia pauni milioni 150 kusuka kikosi chao cha msimu huu. Daley Blind aliepuka kadi nyekundu kwa bahati, baada ya kuonesha dharau kwa mwamuzi akiwa tayari ana kadi ya njano.

Chelsea wanaongoza ligi kwa pointi 26 wakifuatiwa na Southampton wenye 22, Man City 20, Arsenal na West Ham 17 kila moja, Swansea 15, Liverpool 14 sawa na Tottenham ambao jana waliwafunga Aston Villa 2-1.

Everton, Man United, West Brom na Newcastle wanafuatiwa na Stoke wenye pointi 12, Hull 11, Villa 10, Crystal Palace na Leicester tisa, QPR saba na Burnley wanaburuza mkia wakiwa na pointi nne.

Comments