Valdes awazodoa Liverpool

KIPA wa zamani wa kimataifa wa Barcelona, Victor Valdes amewashangaza Liverpool wanaotaka kumsajili, kwa kuwakatalia ofa ya kufanya nao mazoezi ili wabaini utimamu wa mwili wake.
Liverpool wamekuwa wakitajwa kwamba watamsajili kama mchezaji huru baada ya kukataa kuhuisha mkataba wake Barcelona, lakini pia baada ya kuumia vibaya goti msimu uliopita kiasi cha kukaa nje ya dimba kwa muda mrefu.

Kutokana na ukubwa wa majeraha aliyokuwa amepata, ilikuwa busara kwa Liverpool wanaofundishwa na Brendan Rodgers kumjaribu kwanza kabla hawajatiliana saini naye, kwa sababu kuna uwezekano hajapona, akaja kula mshahara bure.

Katika kile kisichotarajiwa na wengi, Valdes, raia wa Hispania, amekataa kwenda kujaribiwa kwa kufanya mazoezi na Liver. Tangu aumie Machi mwaka huu alitakiwa na AS Monaco wa Ufaransa lakini pia akawakataa baada ya Barca pia kumwomba aongeze mkataba akawazodoa.

Haijajulikana hasa Valdes (32) ananuia kuchezea timu gani. Liverpool walitarajia ajitokeze wakati wowote wakimwita ili hatimaye aingie rasmi kwenye kikosi chao, lakini inaelekea itabaki kuwa ndoto ya alinacha.

Mhispania huyo anataka aitwe na kuanguka wino tu kwenye mkataba badala ya kujaribiwa. Ilipata kutokea suala kama hilo Arsenal, miaka kadhaa iliyopita pale Arsene Wenger alipotaka kumsajili Zlatan Ibrahimovic aliyekataa kujaribiwa kwanza, akisema yeye alikuwa wa kusaini tu.

Liver walitaka kumsajili Valdes kama njia ya kumtia shinikizo Simon Mignolet kucheza vyema, kwani msimu huu kiwango chake kimeshuka, tofauti kabisa na msimu uliopita ambapo walikaribia kutwaa ubingwa. Hadi sasa wanashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Valdes amechezea Barcelona mechi zaidi ya 500, akatwaa ubingwa wa Ulaya mara tatu na ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania mara sita.
Nafasi yake Barcelona imechukuliwa na kipa wa Chile, Claudio Bravo aliyeingia Camp Nou akitoka Real Sociedad msimu wa kiangazi.

Comments