Man City safi, Liverpool waamka

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England (EPL), Manchester City wamepata ushindi wa 2-0 dhidi ya Aston Villa, lakini baada ya kubanwa hadi dakika ya 81 ya mchezo.

Villa walioanza ligi vyema kabla ya kufungwa mfululizo, walicheza vizuri na mechi ilikuwa na kila aina ya ushindani, ndipo Yaya Toure alipofanikiwa kuzifumania nyavu dakika ya 82 kwa guu la kushoto baada ya kupata pasi ya Fernando.

Sergio Aguero alimaliza kazi dakika sita baadaye alipopata pasi ya James Milner na kuwapeleka City hadi nafasi ya pili ya msimamo wa ligi japokuwa kubaki hapo itategemea matokeo ya mechi nyingine leo.

Liverpool waliokuwa doro kwenye mechi zilizopita walipata ushindi muhimu dhidi ya West Bromwich Albion, kupitia kwa mabao ya Adam Lallana na Jordan Henderson, huku Saido Beraniho kutoka Burundi akiwafungia West Brom kwa mkwaju wa penati.

Katika mechi nyingine, Sunderland waliwafunga Stoke 3-1, Swansea wakatoshana nguvu ya mabao 2-2 na Newcastle, Hull wakawapiga Crystal Palace 2-0 wakati Leicester na Burnley walitoka pia sare ya 2-2.

Comments