England yataja kikosi

Kocha wa England, Roy Hodgson ametaja kikosi cha wachezaji 21 kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu Euro 2016 zitakazofanyika wiki ijayo dhidi ya San Marino na Estonia.

Katika kikosi hicho, beki wa kulia wa Southampton, Nathaniel Clyne ambaye amecheza vyema kwa Saints wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ameitwa kwa mara ya kwanza.

Kadhalika beki wa kushoto wa Arsenal, Kieran Gibbs na kiungo wa Swansea, Jonjo Shelvey wamo kwenye kikosi hicho. Hata hivyo, beki wa kushoto wa Manchester United ameitwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa U-21.

Daniel Sturridge wa Liverpool hayupo katika kikosi kitakachochuana na San Marino katika Uwanja wa Wembley Alhamisi ijayo kabla ya kwenda Estonia kwa mechi ya Jumapili wiki ijayo.

Washambuliaji kwenye kikosi hicho ni yule wa Arsenal, Danny Welbeck, wa Manchester United, Wayne Rooney na wa Liverpool, Rickie Lambert. Sturridge ameumia, amekosa mechi sita za klabu yake lakini anatarajiwa kurudi dimbani wikiendi hii.

Wengine kwenye kikosi hicho na timu zao kwenye mabano ni makipa Fraser Forster (Southampton), Ben Foster (West Bromwich Albion) na Joe Hart (Manchester City).
Mabeki ni Leighton Baines (Everton), Gary Cahill (Chelsea), Phil Jagielka (Everton) na John Stones (Everton)

Viungo walioitwa ni Fabian Delph (Aston Villa), Jordan Henderson (Liverpool), Adam Lallana (Liverpool), James Milner (Manchester City), Alex Oxlade-Chamberlain (Arsenal), Raheem Sterling (Liverpool), Andros Townsend (Tottenham Hotspur) na Jack Wilshere (Arsenal).

Comments