Newcastle hali tete

Kocha wa Newcastle, Alan Pardew ametiwa katika shinikizo jipya baada ya kuendelea kupoteza mechi.

Washabiki wa Newcastle wamekuwa wakimtaka mmiliki wa klabu, Mike Ashley kumfukuza kocha huyo, kwani timu imo mkiani mwa ligi na hakuna jipya.

Mmiliki huyo alidai kabla ya mechi dhidi ya Stoke kwamba angemfuta kazi Pardew iwapo wangepoteza mechi, lakini baada ya Stoke kuwafunga 1-0, akadai ilikuwa utani tu.
Washabiki waliendelea kubeba mabango yenye maandishi ya kutaka kufukuzwa kwa kocha huyo Mwingereza, mengine yakiwa na picha yake ikifananishwa na katuni tata.
Ujumbe mwingine ulikuwa kwamba wana imani na timu ila kocha hawezi na wengine wakiandika kwamba tatizo la klabu yao ni mmiliki, Ashley.

Bao la kichwa la Peter Crouch limemwelekeza pabaya kocha huyo, ambaye lolote sasa linaweza kumpata, ama kufukuzwa, mwenyewe kung’atuka au kuendelea kuzongwa na washabiki.

Newcastle wanashika nafasi ya 20 miongoni mwa idadi hiyo ya timu kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi tatu kutokana na mechi sita, sawa na Burnley, huku uwiano wa mabao kwa timu zote mbili ukiwa ni -7.

Pardew aliwaambia waandishi wa habari kwamba ataendelea na kazi yake, wala hana mpango wa kujiuzulu, japokuwa shinikizo likizidi ataondoka tu.

Comments