Arsenal kusajili mabeki

Arsenal wameshituka kwamba wanaweza kufanya vibaya wasiporekebisha safu yao ya ulinzi, na wanafikiria kusajili wachezaji wawili.

Baada ya kuumia kwa beki tegemeo wa kulia, Mathieu Debuchy atakayekuwa nje kwa miezi miwili na kukosa mechi karibu 10 za Ligi Kuu, sasa wanaangalia wachezaji huru.

Arsenal wanadaiwa kuwajadili wachezaji kadhaa, akiwamo mlinzi wa zamani wa Everton, Joseph Yobo (34) na beki wa zamani wa kati wa West Bromwich Albion, Diego Lugano (33).

Kuugua mafindofindo beki Calum Chambers na kuumia kidogo Nacho Monreal kuliwaweka Arsenal katika hali mbaya walipokwenda Ujerumani, na huko walirudi na mabao mawili kutoka kwa Borussia Dortmund, bila wao kufunga lolote.

Ni kwa ajili hiyo wanafikiria pia kumchukua kiungo wao wa zamani, Lassana Diarra (29) aliyeachana na Lokomotiv Moscow.

Debuchy alisajiliwa kuziba pengo la Bacary Sagna aliyeondoka kwa mkataba wake kumalizika na kujiunga na Manchester City na hawakusajili beki mwingine wa kati baada ya kumuuza nahodha wao Thomas Vermaelen kwa Barcelona kiangazi hiki.

Walikuwa pia wakihusishwa na kumsajili mchezaji wa Colombia aliyewika kwenye fainali za Kombe la Dunia, Mario Yepes anayefikiria kutundika daluga na kuwa kocha.

Comments