Jerome Champagne kumvaa Blatter

Katibu Mkuu Msaidizi wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Jerome Champagne ametangaza kuwania urais wa kuchuana na Rais Sepp Blatter.

Champagne (56) ambaye ni raia wa Ufaransa amechukua uamuzi huo huku Kiongozi wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), Michel Platini aliyetarajiwa kumkabili Blatter akisema hana nia hiyo tena.

Mwanadiplomasia huyo wa zamani amesema kwamba tayari ameiandikia barua Kamati ya Muda ya Uchaguzi ya FIFA pamoja na Rais wake, Domenico Scala kuthibitisha nia yake ya kuwania nafasi hiyo kubwa zaidi kwenye soka.

Blatter alitangaza wiki iliyopita kwamba atatetea kiti chake, ukiwa ni muhula wa tano. Champagne amefanya kazi FIFA kwa miaka 11 kwenye ngazi ya utendaji kabla ya kung’atuka 2010.

Champagne anahitaji kuungwa mkono na vyama sita vya soka katika nchi mbalimbali, lakini habanwi kuweka hadharani ni vipi hivyo hadi utangazaji rasmi wa kugombea nafasi hizo utakapowekwa wazi Januari mwakani.

Mwaka 2011 Blatter alitangaza kwamba alikuwa na mpango wa kustaafu nafasi hiyo na kwamba hangewania tena kiti hicho kwenye uchaguzi wa mwakani, lakini sasa amebadili uamuzi, hivyo atashiriki kwenye uchaguzi wa Juni.

Champagne anasema kwamba lazima wafanye uamuzi wa wazi na kujihukumu iwapo wanataka kuendelea na ubaguzi wa kiuchumi na kutokuwa na mizania kwenye soka, mambo aliyosema hayakubaliki kwenye karne ya 21 ya utandawazi.

Amesema kwamba miaka 10 ijayo itakuwa muhimu sana kwa soka na maendeleo yake, kwa namna ya pekee kwa FIFA aliyosema ipo njiapanda na inahitaji mabadiliko makubwa ili ifikie mafanikio.

Comments