Man U hasara kubwa

Manchester United wanatarajia kupata hasara kubwa kifedha kutokana na kufanya vibaya kwa wachezaji wake uwanjani.
Klabu hiyo inatarajia kwamba mapato na faida zake katika mwaka ujao yataanguka kwa kiasi kikubwa, kutokana na, pamoja na mambo mengine, kushindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika miaka 20.

Inaelezwa kwamba kipato halisi kimepungua kwa asilimia 84 kwa mwaka ulioishia Juni, ambapo walipata pauni milioni 23 ikilinganishwa na pauni milioni 146 mwaka mmoja tu uliopita wakati akiwapo Sie Alex Ferguson.

Kocha huyo mahiri alistaafu na nafasi yake kuchukuliwa na Mskochi mwenzake, David Moyes ambaye aliwatumbukiza Mashetani Wekundu kwenye moto usiozimika na kuishia nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, wakati ndio walikuwa mabingwa watetezi.

Klabu hiyo ambayo kwa asilimia kubwa inamilikiwa na Familia ya Glazer wa Marekani, inasema kwamba katika mwaka wa fedha wa 2013/14 faida iliongezeka kwa asilimia 19 hadi kufikia pauni £433.2m kutokana na matangazo ya televisheni na udhamini.

Hata hivyo, sasa inatabiri kwamba gaida itashuka kwa kati ya £385m na £395m na faida inatarajiwa kushuka kwa kati ya £90m na £95m. Matokeo yanaonesha pia kwamba Moyes aliyefukuzwa kazi pamoja na benchi lake la ufundi walilipwa fidia ya pauni milioni 5.2 Aprili baada ya kuwa kazini kwa pungufu ya mwaka mmoja.

Hivi sasa United wanaye kocha mpya katika Louis van Gaal ambaye ameanza vibaya kwa kufungwa mechi ya kwanza ya ligi kuu, kwenda sare mechi nyingine mbili na kufungwa 4-0 na timu ya daraja la tatu ya MK Dons na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Ligi.

Hata hivyo, amefanya usajili wa wachezaji wengi wanaodhaniwa watasaidia kuirejesha klabu kwenye hadhi yake na kurudisha kuogopewa hasa wanapocheza kwenye uga wa nyumbani wa Old Trafford.

Comments