Welbeck awabeba England

England wamepata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uswisi kupitia kwa mshambuliaji mpya wa Arsenal, Danny Welbeck katika mechi za kufuzu kwa michuano ya Euro 2016.

Yalikuwa mabao yake ya kwanza kwa timu hiyo katika kipindi cha mwaka mzima, ambapo kipa Joe Hart na beki Garry Cahil walicheza vizuri katika kikosi cha Roy Hodgson na kuwanyima wenyeji ushindi au sare.

Welbeck aliyenunuliwa na Arsenal kutoka Manchester United siku ya mwisho ya usajili wa majira ya joto alifunga bao la kwanza dakika ya 58 baada ya kutiliwa mpira na Raheem Sterling wa Liverpool

Wakati mpira ukielekea kumalizika, Welbeck alifunga bao la pili baada ya kupata pasi kutoka kwa Rickie Lambert wa Liverpool, huku kocha Hodgson akifurahia matokeo na kusema kwamba England wapo katika mwelekeo sahihi.

Nusura Uswisi wafunge kama si kipa Hart kujitahidi na kutibua mpira kwa mguu ambao ulishamshinda kudaka na pia Cahil alisafisha mpira uliokuwa kwenye mstari wa goli ukiingia kwenye nyavu.

Ngome ya England bado ilionekana kuyumba nyakati fulani, hasa kwa Phil Jones lakini watajirekebisha kadiri muda unavyokwenda, maana mechi hii ndiyo ilichukuliwa kuwa ngumu zaidi kwa sababu zijazo ni dhidi ya San Marino, Estonia, Lithuania na Slovenia.

Katika mechi nyingine Jumatatu hii, Luxembourg walikwenda sare ya 1-1 na Belarus, Hispania wakawakandika Macedonia 5-1, Ukraine wakalala 1-0 mbele ya Slovakia na Estonia wakawashinda Slovenia 1-0.

Matokeo zaidi katika mechi hizi za kwanza za kufuzu kwa Euro 2016 San Marino walilala 2-0 mbele ya Lithuania, Urusi wakawachakaza Liechtenstein 4-0, Austria wakatoshana nguvu na Sweden kwa bao moja moja wakati Montenegro waliwazidi nguvu Moldova kwa 2-0.

Comments