Van Persie amwonya Falcao

Mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie amemwonya mchezaji mpya wa timu hiyo, Radamel Falcao kwamba lazima agombanie namba.

Falcao aliyesajiliwa katika siku ya mwisho ya Dirisha la Usajili kwa mkopo kutoka Monaco ya Ufaransa kwa pauni milioni sita, anacheza nafasi moja sawa na Van Persie na nahodha wao, Wayne Rooney.

Usajili wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia ulishangaza wengi, kwani United walitarajiwa kuimarisha maeneo ya beki badala ya ushambuliaji, eneo ambalo wapo vizuri.

Van Persie amesema kwamba hata yeye anapigana kuhakikisha anakuwa chaguo la kwanza mbele ya kocha Louis van Gaal na kwamba timu kubwa kama Man U ni vyema kuwa na wachezaji wa kiwango cha juu kama ilivyo kwenye washambuliaji hao.

“Napokea vyema ujio wake, atatufanya tuwe wazuri zaidi. Klabu kubwa lazima zitafute wachezaji bora zaidi inayoendana na falsafa yangu. Falcao lazima apiganie namba sawa na mimi,” akasema Mdachi huyo aliyesajiliwa misimu miwili iliyopita kutoka Arsenal.

Falcao (28) alifunga mabao 11 katika mechi 20 msimu uliopita kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa kabla ya kuumia goti Januari kiasi cha kumkosesha fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.

Persie (31) inasemakana tayari wanagombea namba na Rooney na zilizuka tetesi majuzi kwamba anaumwa goti ambalo angefanyiwa upasuaji hivi karibuni.

RVP alikanusha madai hayo, akasema anafurahi jinsi watu wanavyoweza kubuni jambo kama hilo, akisema hajui wanatoa wapi, na kwamba hatarajii kwenda kwenye hospitali yoyote ile kwa ajili ya upasuaji.

Comments