Rojo wa Man U ruksa kucheza

Hatimaye mlinzi mpya wa Manchester United, Marcos Rojo ameruhusiwa kuichezea klabu hiyo.
Rojo (24) aliyesajiliwa zaidi ya wiki mbili zilizopita kutoka Sporting Lisbon ya Ureno, hakuweza kucheza kwa sababu Uingereza haikuwa imempatia kibali cha kufanya kazi nchini.

Aliingia kwa viza ya kitalii, akakosa ya kufanya kazi kwa sababu Uhamiaji bado walikuwa wakifuatilia shauri lake la jinai nchini mwake, Argentina.

Rojo aliyesajiliwa kwa pauni milioni 16 anadaiwa kupigana na jirani yake jijini Buenos Aires, Argentina na sasa shauri lake linakaribia kupelekwa mahakamani.

Hata hivyo, hilo halitamzuia kucheza, na hata akitiwa hatiani anaweza kuhukumiwa kufanya kazi za jamii, anazoweza kuzifanya hapo Manchester.

Kocha Louis van Gaal alithiriwa kwa kumkosa kwenye mechi zote zilizopita ambapo United hawajashinda hata moja.

Walifungwa 2-1 na Swansea, kwenda sare 1-1 na Sunderland na kutoka suluhu na Burnley katika mechi za Ligi Kuu ya England, wakati MK Dons waliwafyatua Mashetani Wekundu 4-0 na kuwatupa nje ya Kombe la Ligi.

Van Gaal amechukua hatua za kusajili wachezaji kadhaa, wakiwamo Angel Di Maria kwa pauni milioni 60 akivunja rekodi ya Uingereza, Daley Blind, Radamel Falcao na wengineo.

Rojo alitamba na Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil na anatarajiwa atasaidia ngome ya United inayotetereka baada ya kuondoka kwa akina Patrice Evra, Rio Ferdinand na Nemanja Vidic.

Comments