Arsenal sare tena

Arsenal wameambulia pointi moja katika safari yao kwa Leicester, timu iliyopanda daraja msimu huu.
Mchezaji mpya wa Arsenal, Alexis Sanchez alifunga bao dakika ya 20, lakini dakika mbili baadaye Leonardo Ulloa akasawazisha baada ya kupanda juu zaidi ya Laurent Koscielny na kufanya sare.

Sanchez amefunga bao la pili katika mashindano muhimu, hili likiwa ni la kwanza kwa ligi katika mechi tatu, jingine alifunga kwenye mechi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi ya Besiktas ya Uturuki.

Bao la Sanchez lilikuja baada ya Yaya Sanogo kuwa amejaribu kumvukisha kipa Kasper Schmeichel, na Arsene Wenger anasema kwamba raia huyo wa Chile anaweza kuvaa viatu vya Olivier Giroud aliyeumia na atakuwa nje kwa miezi kati ya mitatu au minne, japokuwa kuna tetesi za kuwasili mshambuliaji mwingine Jumatatu hii.

Leicester walicheza vyema na inabidi Arsenal wajipange vizuri zaidi kwa ajili ya mechi zinazokuja, kwa sababu hii ni sare ya pili baada ya mechi iliyopita kutoshana nguvu 2-2 na Everton ugenini, lakini mechi ya kwanza waliwafunga Crystal Palace 2-1 kwa tabu nyumbani Emirates.

Vijana wa Nigel Pearson waliendelea na kasi yao na nusura kipindi cha pili wapate mabao zaidi, kama si Ulloa na mchezaji aliyetokea benchi, Jamie Vardy kukosea, na pia kipa wa Arsenal, Wojciech Szczesny kuokoa, hivyo kuwapa ahueni vijana wa London Kaskazini.

Comments