Sanchez awavusha Arsenal

Arsenal wamefanikiwa kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa mwaka wa 17 mfululizo, kutokana na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Besiktas kwenye Uwanja wa Emirates, jijini London.

Alikuwa mchezaji mpya kutoka Barcelona kwa pauni milioni 35, Alexis Sanchez aliyepambana na kuwaamsha vitini washabiki wa Arsenal kwa bao lake safi la dakika ya 45. Kwenye mechi ya awali nchini Uturuki, timu hizo zilikwenda suluhu.

Arsenal walimaliza mechi wakiwa mchezaji mmoja pungufu kutokana na beki wa kulia, Mathieu Debuchy kupewa kadi nyekundu dakika ya 75na pia waliwakosa nahodha Mikel Arteta na mshambuliaji, Olivier Giroud walioumia na kiungo mahiri, Aaron Ramsey aliyekuwa na kadi mbili za njano.

Kocha Arsene Wenger amemsifu Sanchez, akisema alipambana na kuonesha dhamira ya kutochoka na kiungo Jack Wilshere naye alionesha vitu adimu uwanjani hapo, huku Wenger akiweka vyema rekodi yake ya kufuzu, kitu alichokuwa amekidhamiria sana msimu huu.

Arsenal walionesha kuwa wazuri kwenye ulinzi, safu ikiongozwa na nahodha msaidizi, Per Mertesacker, Debuchy, Nacho Monreal na Laurent Koscielny, kabla ya chipukizi Calum Chambers kuingia baadaye kipindi cha pili kuiimarisha zaidi.

Wenger sasa amebaki kutoa uamuzi iwapo atasajili mshambuliaji mpya kwa sababu Giroud atakuwa nje kwa miezi mine baada ya kuvunjika mguu au ataendelea kuwatumia wlaiopo; Sanchez, Yaya Sanogo, Lukas Podolski na Joel Campbell.

Zipo habari kwamba anataka kusajili mshambuliaji mmoja kati ya Danny Wellbeck, Edinson Cavani au Loic Remy, lakini Manchester United hawataki kuuza, na pia yeye aliwakatalia kuwauzia Thomas Vermaelen, Cavani ni ghali sana, kwenye pauni milioni 50 na Remy anaweza asiwe na uwezo kuwashinda waliopo sasa.

Comments