Di Maria: Man United kutoa £75m?

Manchester United watalazimika kuvunja rekodi ya madau ya usajili kwa Uingereza, ili kumpata winga wa Argentina anayetaka kuondoka Real Madrid, Angel Di Maria.

Kocha wa Real, Carlo Ancelotti amebainisha kwamba baada ya Di Maria kukataa mkataba mpya Santiago Bernabeu, ameruhusiwa kuondoka na kwamba Jumapili hii amewaaga wenzake.

Inaelekea kwamba atajiunga na Manchester United, lakini Real Madrid wamewaeleza United kwamba ikiwa wanamtaka lazima watoe pauni milioni 75, kiwango ambacho hakijapata kutolewa na klabu yoyote nchini Uingereza.

Man U, hata hivyo, wanaamini kwamba dau hilo litashuka labda hadi pauni milioni 50, sawa na zile ambazo Chelsea walitumia kumnunua Fernando Torres kutoka Liverpool mwaka 2011. Torres sasa ni chaguo la tatu kwenye mshambuliaji wa kati, lakini Kocha Jose Mourinho amesema angependa abaki Stamford Bridge.

Mara ya mwisho Man United walivunja rekodi ya Uingereza mwaka 2002 walipotoa pauni milioni 29.1 kwa kumsajili beki wa kati, Rio Ferdinand. Ancelotti alisema kwamba Di Maria hakufanya mazoezi Jumapili hii, bali alifika kuwaaga wachezaji wenzake japokuwa bado si rasmi kwamba anaondoka.

“Hakuna chochote rasmi bado lakini jambo hili linashughulikiwa. Ni juu yake na klabu imefanya kila lililoweekana kumbakiza hapa. Hakufanya mazoezi nasi leo, ila alikuja kuaga,” alisema Ancelotti.

Kocha wa Man United, Louis van Gaal anatambulika kutaka aina ya uchezaji wa Di Maria kwenye wingi kwa sababu ya kasi na uwezo wake wa kumiliki mpira vinavyohitajika Old Trafford, hivyo huenda asisite kumwaga kitita kizito.

Habari nyingine zinasema kwamba wakala wa Di Maria aliondoka Hispania mapema Jumapili kutua London kwa ajili ya mazungumzo. Habari nyingine zinasema kwamba Sami Khedira, kiungo wa Real Madrid ameamua kubaki klabuni hapo, licha ya kutakiwa na klabu kadhaa kama Arsenal na Chelsea.

Comments