Rwanda waeunguliwa Afcon

*Ni kwa utambulisho tata wa mchezaji

Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon) imewaondoa Rwanda kwenye timu zilizofuzu kushiriki fainali za Morocco mwakani, baada ya kubainika kwamba mchezaji wao alighushi uraia wa nchi hiyo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kamati kupitia malalamiko ya Shirikisho la Soka la Kongo (Fecofoot) juu ya mchezaji Birori Dady aliyecheza kwenye mechi ya mkondo wa kwanza Julai 20 mwaka huu mjini Pointe-Noire.

Imebainika kwamba pasi ya kusafiria ya mchezaji huyo wa AS Vita Club ya Kinshasa, Kongo inasomeka Etekiama Agiti Tady, na pia umri wake ni tofauti. Uchunguzi wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa kupokea nyaraka kutoka mashirikisho ya Rwanda, Kongo Brazzaville na Kongo Kinshasa, imebainika kwamba vitu vyote hivyo vinahusiana na mtu huyo huyo.

Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) lilishikilia kwamba wanajua Dady Birori ana utambulisho mmoja lakini uchunguzi zaidi umebaini kwamba alipoitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa na Derwafa, lilitumika jina la Etekiama Agiti Tady.

Kwa kuzingatia kanuni za mashindano hayo, Kamati ya Maandalizi imewaengua Rwanda kwenye mashindano hayo na kuwavusha Kongo Brazzaville, kumsimamisha mchezaji huyo (Etekiama Agiti Tady / Birori Dady) dhidi ya kuchezea klabu na timu ya taifa hadi itakapoamuliwa vinginevyo.

Kadhalika Rwanda wametangazwa kuwa walipoteza mechi yao dhidi ya Kongo na kuondoshwa kwenye amshindano, na sasa Kongo wanaingizwa kwenye hatua za makundi ya Orange Africa Cup of Nations – Morocco i2015 katika Kundi A kuchukua nafasi ya Rwanda.

Caf imesema inayo mamlaka ya kuthibitisha muda wa kifungo dhidi ya mchezaji huyo na pia kuongeza adhabu zaidi ikibidi wakati wa kikao kijacho cha Kamati ya Maandalizi Septemba 17 mwaka huu. Imewataka wachezaji kuweka sawa mambo yao ikiwa wana utambulisho zaidi ya mmoja.

Comments