Liverpool washinda kwa mbinde

Liverpool wameanza maisha bila Luis Suarez katika Ligi Kuu ya England kwa tabu, ambapo walibanwa na Southampton, lakini wataridhika na ushindi wa mabao 2-1 waliopata.

Wakiwa pia wamewapora Southampton wachezaji watatu nyota, Liverpool walitarajiwa kung’ara, lakini karibu muda wote wa mchezo walikuwa hatarini, na licha ya kuongoza kupitia kwa Raheem Sterling dakika ya 23, Saints walisawazisha.

Washabiki dimbani Anfield hawakujihisi kwamba ni timu yao inacheza nyumbani, kwani tofauti na msimu uliopita ambapo walimaliza ligi nafasi ya pili baada ya kuteleza kidogo kuutwaa ubingwa, walibanwa maeneo mengi.

Saints walisawazisha bao kupitia kwa Nathaniel Clyne katika dakika ya 56, lakini halikudumu sana, kwani Daniel Sturridge, mshirika wa msimu uliopita wa Luis Suarez katika kucheka na nyavu aliwapatia Reds bao la ushindi dakika ya 79.

Liverpool wamewanyakua Rickie Lambert, Adam Lallana na  Dejan Lovren kutoka Southampton katika mpango wa usajili ambapo hadi sasa wameshatumia zaidi ya £100m kujiboresha na kuziba pengo la Suarez. Lovren na Lambert walicheza mechi hiyo, Lambert akiingia kipindi cha pili.

Hata hivyo, Saints walicheza vyema chini ya kocha wao mpya, Ronald Koeman, ambapo kipa Fraser Forster; beki wa kushoto, Ryan Bertrand; kiungo mchezeshaji Dusan Tadic; mshambuliaji Graziano Pelle na kiungo Morgan Schneiderlin walicheza vyema na huenda timu ikafanya vyema msimu huu tofauti na ilivyotarajiwa.

Comments